Breaking News

SIMBA WAFANYA KUFURU, HAYA HAPA MAJINA MATANO ALIYOKABIDHIWA MO

SIMBA WAFANYA KUFURU, HAYA HAPA MAJINA MATANO ALIYOKABIDHIWA MO

Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, tayari ana majina ya wachezaji watano aliopendekeza wasajiliwe ambayo tayari ameyakabidhi kwenye bodi ya timu hiyo iliyopo chini ya mfadhili wake, bilionea, Mohammed ‘Mo’ Dewji.

Mbelgiji huyo anataka kuwasajili wachezaji hao katika usajili huu wa Ligi Kuu Bara uliofunguliwa Novemba 15, kabla ya kufungwa Desemba 15, mwaka huu.

Kocha huyo, hivi karibuni alitaja nafasi anazotaka kuzisajili katika kukiimarisha kikosi chake ambazo ni safu ya kiungo mkabaji, winga na mshambuliaji mmoja, wote wenye uzoefu.

Imeelezwa kati ya majina hayo matano, kocha huyo atawasajili wachezaji watatu pekee baada ya kuridhishwa na viwango vyao.

Mtoa taarifa huyo alisema, kati ya wachezaji hao watano wapo wazawa aliowaona kwenye mzunguko huu wa kwanza wa ligi na wengine wa kutoka nje ya nchi.

“Kocha tayari ana majina yake ya wachezaji watano, kati ya hayo matatu ndiyo atayapitisha kwa ajili ya kusajiliwa baada ya kuwachuja na kuikabidhi ripoti yake ya usajili kwa bodi.

“Baada ya kukabidhi majina hayo, Bodi ya Simba imepanga kukutana kwa ajili ya kupitia majina hayo kwa ajili ya kuwasajili katika usajili huu wa dirisha dogo.

“Uongozi umepanga kufanya usajili wake kwa ripoti ya kocha ili baadaye kuepukana na lawama pale ikifanya vibaya katika ligi na michuano ya kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo.

Kwa upande wa Simba, mwenyekiti wa bodi hiyo, Swedy Mkwabi, alizungumzia hilo na kusema: “Kila kitu kinakwenda vizuri katika timu, lakini kuhusiana na usajili, suala lipo kwa kocha ambaye tumempa jukumu la kusimamia usajili huo.

“Na kikubwa hatutaki kumuingilia katika masuala hayo ya usajili na tumepanga kufanya usajili kwa kufuata ripoti ya kocha aliyoikabidhi kwa kamati husika, hivyo tusubirie kama masuala hayo ya usajili yakikamilika basi kila kitu tutaweka wazi.

No comments